IQNA

Mamillioni duniani washiriki maombolezo ya Imam Hussein AS

18:19 - August 30, 2020
Habari ID: 3473117
TEHRAN (IQNA)- Mamillioni ya watu kote duniani wameshiriki katika maombolezo ya mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS, ambaye aliuawa katika siku kama ya leo ambayo ni maarufu kama Ashura.

Katika siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria, katika hali ambayo, majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo kwa Swala na kunong'ona na Mola wake.

Usiku huo Imam Hussein aliwakusanya wafuasi wake na baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume, aliwaambia: ''Kila anayetaka, aitumie fursa iliyobakia ya giza la usiku kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake, kwani hakuna atakayebaki hai hapo kesho tutakapokabiliana na jeshi la Yazid.'' Hata hivyo masahaba na wafuasi waaminifu na waumini wa kweli wa mtukufu huyo walikuwa wameshakata shauri la kujitolea mhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hadi tone la mwisho la damu zao. Usiku huo wa kuamkia Ashura yaani tarehe 10 Muharram, uwanja wa Karbala ulikuwa medani ya ibada kwa mashujaa ambao licha ya kuwa wachache kwa idadi lakini walisimama imara kama mlima na hawakumuacha Imam na kiongozi wao hata dakika moja.

Kwa mnasaba wa siku hii mwaka huu, pamoja na kuwepo janga la COVID-19, Waislamu na wasiokuwa Waislamu wameshiriki katika maombolezo kwa kuzingatia kanuni za kiafya.

Katika tukio la Karbala lililojiri katika siku kama ya leo, Imam Hussein AS, Imamu wa Tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani alisisitiza na kueleza bayana kwamba: "Kusudio langu ni kuufichua na kuufedhehesha utawala ulio dhidi ya Uislamu, kuamrisha mema na kukataza mabaya na kukabiliana na dhulma na uonevu."

Mafunzo ya harakati ya Imam Hussein AS yamesambaa na kutanda katika historia na jiografia ya viumbe, wanadamu na ulimwengu mzima na hayawezi katu kuishia kwenye mipaka maalumu.

3472408

Kishikizo: imam hussein as ashura
captcha