IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Vyama vote viwili Marekani huiletea Iran shari

22:47 - November 16, 2016
Habari ID: 3470680
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikishuhudia uadui kutoka kwa vyama viwili vikuu vya Marekani.
Ayatullah Seyyed Ali Khamenei ameyasema hayo leo hapa Tehran  alipohutubia hadhara ya maelfu ya wananchi kutoka mkoa wa Isfahan katikati mwa Iran. Ameashiria mjadala uliojitokeza katika kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani kuhusu matatizo na hali halisi ya ndani ya jamii ya nchi hiyo na kusema: Mtu aliyechaguliwa kuwa Rais Marekani alisema katika kampeni za uchaguzi kwamba, lau kama fedha zilizotumiwa na nchi hiyo katika miaka kadhaa iliyopita kwa ajili ya vita zingetumika kwa ajili ya masuala ya ndani ya Marekani tungeweza kuijenga upya nchi hii". Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amehoji kuwa, je watu waliopumbazwa na nukta hiyo bandia wanaelewa maana ya maneno haya?

Ayatullah Khamenei amegusia pia mijadala iliyotawala kampeni za uchaguzi wa rais nchini Marekani kuhusu uharibifu, umaskini na matatizo mengi yaliyopo nchini humo na kusema: katika miaka ya hivi karibuni Marekani imetumia fedha za watu wa nchi hiyo katika vita visivyokuwa sharifu na matokeo yake ni mauaji ya makumi ya maelfu ya raia na kuharibiwa miundombinu katika nchi kama Afghanistan, Iraq, Libya, Syria na Yemen.

Vilevile ameashiria matokeo ya uchaguzi wa rais wa Marekani na kusema: Iran haina hukumu ya aina yoyote kuhusu uchaguzi huo kwa sababu Marekani bado ni ileile na chama chochote kilichoshika madaraka nchini humo katika kipindi cha miaka 37 iliyopita kati ya vyama viwili vya Republican na Democratic hakikuwa na kheri kwetu sisi na daima shari yao imekuwa ikilifikia taifa la Iran.

Ayatullah Khamenei amesema kinyume na baadhi ya watu duniani ambao wamepatwa na majonzi kutokana na matokeo ya uchaguzi wa rais wa Marekani au wale wanaofurahia matokeo hayo, sisi hatuko kwenye msiba wala hatuyafurahii kwa sababu hakuna tofauti kwetu sisi na wala hatuna wasiwasi, na kwa baraka zake Mwenyezi Mungu tuko tayari kukabiliana na lolote linaloweza kutokea. 

3546535


captcha