IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran inapaswa kuimarisha uwezo wake kukabiliana na maadui

18:44 - December 27, 2016
Habari ID: 3470763
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatollah Ali Khamenei amesema Iran inapaswa kuendelea kuimarisha nguvu zake ili kukabiliana na maadui.
Iran inapaswa kuimarisha uwezo wake kukabiliana na maadui

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo wakati akihutubu leo Jumanne mjini Tehran katika mkesha wa maadhimisho ya kufanyika maandamano makubwa ya kuunga mkono mfumo wa Kiislamu kote Iran mnamo Disemba 30, 2009 maarufu kama Hamas ya Tisa Dey.

Kiongozi Muadhamu akihutubu katika darsa yake ya fiqhi ameyataja maandamano hayo kuwa mfano wa nguvu na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei amesema hakuna yeyote aliyesimamia maandamano hayo bali wananchi wenyewe walijitokeza kutokana na uwezo wao wa kifikra ambao ni moja ya nguzo za mfumo wa Kiislamu. Ameashiria pia Hadithi ya Mtume Muhammad SAW kuwa kupatikana saada na kheria katika jamii ya mwanadamu kunawezekana kwa sharti la kuwa na nguvu na uwezo. Ameongeza kuwa, madola ya Kiistikbari kama vile Marekani yanalenga kueneza satwa na kupora utajiri wa maeneo mengine duniani kwa msingi wa kile wanachokitaja kuwa ni "thamani za Kimarekani."

Kwingineko katika matamshi yake, Kiongozi amesema: "Leo, madola  ya kiistikbari yanalenga kuipokonya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uwezo wake wa kimaada na kimaanawi pamoja na irada yake. Kwa msingi huo tunapaswa kulinda na kuimarisha uwezo wetu wote siku hadi siku."

Ayatullah Khamanei amesema uhasama na njama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ni kutokana na nchi hii kupinga vikali mfumo wa ubeberu duniani.

Hali kadhalika katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelaani umiliki na utumizi wa silaha za nyuklia kwa kusema: "Uharamu wa silaha za nyuklia una misingi muhimu ya kifiqhi na kifikra. "Wakati huo huo amesema serikali na taifa la Iran linapaswa kujitahidi kumiliki aina nyinginezo za nguvu za kujihami.

Ayatullah Khamenei amewahi kutoa fatwa ya kuharmisha umiliki na utumizi wa silaha za nyuklia.

3557139

captcha