IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Waislamu waungane kukabiliana na ufarakanishaji wa mabeberu

10:51 - December 18, 2016
Habari ID: 3470747
IQNA: Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, daima Uingereza imekuwa chimbuko la vitisho, ufisadi na mabalaa kwa eneo la Magharibi mwa Asia.

Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo Jumapili hapa mjini Tehran alipokutana na wageni walioshiriki Mkutano wa 30wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu hapa Tehran na watu wa matabaka mbalimbali ya wananchi na kubainisha kwamba, hii leo kuna irada mbilizinakabiliana katika Mashariki ya Kati, irada ya umoja na irada ya kufarakanisha.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, katika mazingira haya nyeti kuegemea Qur'ani tukufu na mafundisho ya Mtume SAW ndio dawa ya umoja kwa ajili ya kutibu na kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayoukabili Ulimwengu wa Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria siasa na hatua za Waingereza katika karne mbili za hivi karibuni na kuzitaja kuwa chimbuko la shari na mabalaa kwa mataifa ya eneo la Asia ya magharibi na kukumbusha kwamba, hivi karibuni, Waingereza bila haya wala soni na katika hatua ya aibu kabisa, wamelituhumu taifa madhulumu la Iran kwamba, eti ni tishio kwa eneo la Mashariki ya Kati, ilihali watu wote wanajua kwamba, kinyume na tuhuma hizo, ni Waingereza ambao daima wamekuwa chimbuko la vitisho, ufisadi, hatari na mabalaa.

Ayatullah Khamenei sambamba na kukumbusha njama za kila leo za ubeberu na ukoloni za kuzusha mifarakano na kutaka kuwadhoofisha Waislamu, ameongeza kuwa, hii leo Ulimwengu wa Kiislamu umekumbwa na masaibu na taabu nyingi na kwamba, njia ya kukabiliana na hayo ni kuweka kando hitilafu za kimadhehebu na kudumisha umoja na mshikamano.

3554453

captcha