IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Juhudi zaidi zifanyike kuitambulisha Swala ipasavyo

0:16 - December 09, 2016
Habari ID: 3470727
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuna haja ya kufanyika hima na juhudi za kuifahamu na kuitambulisha Swala katika nafasi yake inayostahiki na amali za mtu binafsi ziendane nayo.

Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo Alhamisi katika ujumbe maalumu alioutuma kwa Kongamano la 25 la Kitaifa  la Swala  nchini Iran na kusisitiza kwamba, Swala ni mlango ulio wazi kwa umma wote ambao unaweza kuutumia  kwa ajili ya kufikia uongofu na rehma za Mwenyezi Mungu na wakati huo huo, kuyaelekeza maisha upande sahihi uliojaa kheri na baraka.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika ujumbe wake huo uliosomwa kwa niaba yake na Hujjatul Islam Walmuslimiin Sayyed Husseini Hamedani, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala katika mkoa wa al-Borz ambaye pia ni Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Karaj magharibi mwa Tehran kwamba, usalama wa kiroho wa kila mtu unafungamana na ibada ya Swala na njia nyoofu pamoja na maisha mazuri ya jamii nayo yanapatikana kupitia kusimamisha ibada ya Swala.

Ayatullah Khamenei amesisitiza katika risala yake hiyo kwamba, sisitizo la Qur'ani Tukufu na Suna juu ya kusimamishwa Swala halina lengo jingine ghairi ya kuwa, mlango wa rehma kwa mtu binafsi na jamii ya Waislamu uko wazi siku zote.

Amekumbusha pia kuwa, viongozi wa serikali, wanazuoni, wasimamizi wa tablighi na mafunzo ya dini na watu wa matabaka yote katika jamii, wote wana masuuliya na jukumu la pamoja katika kusimamisha Swala.

3552165


captcha