IQNA

Bajeti ya Kenya yafungua njia ya mfumo wa kifedha wa Kiislamu

12:00 - April 04, 2017
Habari ID: 3470918
TEHRAN (IQNA)-Serikali ya Kenya imezindua bajeti ambayo itastawisha mfumo wa Kiislamu wa kifedha nchini humo kwa lengo la kuufanya mji mkuu, Nairobi kuwa kitovu cha sekta hiyo kieneo.

Bajeti hiyo iliyozinduliwa Aprili 3 katika bunge la kitaifa inaweza kuleta msukumo mpya katika sekta ya mfumo wa Kiislamu wa banki ambao uemkuwa ukitumika nchini Kenya kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Kwa mujibu wa hatua hizo zilizhochukuliwa kama sehemu ya bajeti ya mwaka 2017/2018, Waziri wa Fedha Kenya Henry Rotich amependekeza sheria zenye kuleta usawa katika banki za Kiislamu na banki zinginezo ambazo hutoza riba.

Aidha mabadiliko katika Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma utaiwezesha serikali kutoa noti za Kiislamu za dhamana yaani sukuk au Islamic bonds kama njia mbadala ya kufadhili miradi ya maendeleo ya serikali. Sukuk zinatazamiwa kuwa na mchango mkubwa kuziba pengo la nakisi ya bajeti ya Kenya inayokadiriwa kuwa Ksh bilioni 524.2 ($5.10 billion).

Utekeelzwaji wa mabadiliko hayo unatazamiwa kuanza mara moja kwani sheria husika tayari zimeshaandikwa na Kurugenzi ya Mradi wa Kifedha wa Kiislamu Kenya (PMO) ambayo inaongozwa na Shirika la Kimataifa la Kutoa Ushauri na Dhamana Kuhusu Huduma za Kifedha za Kiislamu (IFAAS).

Mkurugenzi mkuu wa IFAAS Farrukh Raza amesema lengo la serikali ya Kenya ni kuandaa mazingira ya sukuk na pia kuvutia wawekezaji wa kimataifa.

Wizara ya Fedha imesema inatafakari kuanza kuuza sukuk mwaka huu ingawa uchaguzi mkuu unaofanyika Agosti unaweza kuchelewesha mipango hiyo. Hatua hiyo inatazamiwa kuimarisha nafasi ya Kenya kama kitovu cha mfumo wa fedha wa Kiislamu barani Afrika.

Kwa mujibu wa sheria hizo mpya banki mbili kamili za Kiislamu na pia banki za kawaida ambazo zina huduma za Kiislamu hazitatozwa ushuru unaotozwa banki zenye riba.

Hivi karibuni pia rais wa Kenya alisaini na kuidhinisha Sheria ya Bima (iliyorekebishwa) ya mwaka 2016 ambayo kimsingi itapalekea mashirika ya bima ya Kiislamu yaani Takaful kufanya kazi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na hivyo kuhimiza mashirika ya kimataifa kuwekeza katika sekta hiyo.

Hatua inakuja wiki moja baada ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Kenya (CMA) kuruhusiwa na Baraza la Bodi ya Huduma za Kifedha za Kiislamu (IFSB) kuwa mwanachama wa bodi hiyo. IFSB ina makao yake huko Kuala Lumpur Malaysia na ni bodi ya kimataifa inayoweka viwango na kustawisha huduma za kifedha za Kiislamu zenye uwazi na usimamizi bora duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa CMA Paul Muthaura anasema hatua ya mamlaka hiyo kujiunga na IFSB ni muhimu katika kustawisha Kenya kama kitovu cha huduma za kifedha za Kiislamu eneo la Afrika Mashariki. Amesema hatua hiyo ni kati ya misingi muhimu ya kuufanya mji wa Nairobi uwe kituo cha kimataifa cha kifedha. "Kenya imekuwa ikiweka misingi ya kuwa kitovu cha huduma za kifedha na moja ya sekta ambazo zinazingatiwa na kuifanya nchi hii iwe kitovu cha mfumo wa kifedha wa Kiislamu,” aliongeza.

captcha