IQNA

Kiongozi wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrallah

Marekani ni chanzo cha matatizo eneo la Asia Magharibi

18:47 - August 04, 2023
Habari ID: 3477378
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema Marekani ndiyo sababu ya matatizo mbalimbali ya kiusalama na kiuchumi yanayozisumbua nchi za eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Sayyid Hassan Nasrallah amesema hayo katika hotuba yake iliyorushwa mubashara kwenye runinga kutoka Beirut jana usiku, akihubutia kikao cha kumkumbuka na kumuenzi mwanachuoni wa Kiislamu, marhum Sheikh Afif al-Nabulsi.

Amesema sera za uingiliaji mambo za Marekani ndio mzizi wa changamoto zinazolikumba eneo hili na kuongeza kuwa, utamaduni wa kujikomba kwa Marekani umeyazidishia matatizo mataifa ya eneo. 

Sayyid Nasrallah ameshiria uwepo wa  vikosi vya kigeni katika eneo na kusisitiza kuwa, vikosi hivyo vamizi havisaidii chochote kwa usalama wa Mashariki ya Kati bali ni chanzo kikuu cha mizozo na migogoro katika eneo hili.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameilaumu Marekani kwa matatizo ya umeme yanayoisumbua Lebanon, hali mbaya ya Palestina na matatizo yote yanayowakumba wananchi wa Syria kutokana na vikwazo vya kikatili vya Washington.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sayyid Hassan Nasrullah amesema Marekani inahusika moja kwa moja na inapasa kubebeshwa dhima kwa matatizo yanayowasumbua wananchi wa Yemen akisisitiza kuwa, Washington imekuwa ikizuia jitihada zozote za kurejesha uthabiti katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu.

Kadhalika kiongozi huyo wa kidini na kisiasa wa Lebanon amelaani hatua ya Marekani ya kuizuia Iraq isiilipe Iran deni lake la mabilioni ya dola yanayotokana na mauzo ya gesi asilia na mafuta.

4160030/

captcha